Zaidi ya karne moja tangu meli ya Titanic ilipozama katika safari yake ya kwanza, ushuhuda huu wa mtu wa kwanza aliyenusurika Frank Prentice unasalia kuwa ushahidi muhimu na wa kuogofya kwa waliokuwa ndani ya meli hiyo.

Frank Prentice alikuwa na umri wa miaka 23 aliponusurika katika ajili ya meli ya Titanic iliyozama.

Alipohojiwa na BBC miaka 67 baadaye, ilikuwa wazi bado alikuwa akiandamwa na usiku huo mbaya. Zaidi ya watu 1,500 walikufa maji wakati meli ya Titanic ilipogonga jiwe la barafu katika Bahari ya Atlantiki tarehe 14 Aprili 1912, na kusababisha meli hiyo kuzama.

Bwana Prentice alikuwa akifanya kazi kama msaidizi wa masuala ya fedha, akishughulikia pesa na vifaa ndani ya meli katika safari yake ya kwanza.

Akizungumzia matukio ya usiku huo kwenye kipindi cha hali halisi cha BBC cha 1979 The Great Liners, alikumbuka wakati ambapo alifikiria kwa mara ya kwanza kuwa kuna kitu kibaya kimetokea.

"Hakukuwa na athari sana," alisema. "Ilikuwa ni kama kufunga breki zako kwenye gari na hivyo ndivyo ilivyokuwa - ilisimama. Tulikuwa na mlango wazi na nikatazama nje na anga lilikuwa safi, nyota zilikuwa ziking'aa, bahari ilikuwa imetulia sana na nikajaribu kufikiria lakini singeweza. sikuelewi."

Bwana Prentice alipotoka kwenye eneo lake kwenda nje kwenye sitaha ili kuchunguza, aliweza kuona barafu lakini hakukuwa na dalili ya kilima cha barafu au uharibifu wowote juu ya njia ya maji. Chini ya uso, hata hivyo, uharibifu wa meli iliyodhaniwa kuwa haiwezi kuzama ulikuwa mbaya sana.

Agizo likatolewa kwa wanawake na watoto kuingia kwenye boti za kuokoa maisha, lakini Bw Prentice alisema kuna sababu mbili zilizowafanya wengi kusitasita: ilikuwa ni kina cha futi 70 (21.3m) ndani ya maji, na hawakuwahi kufikiria kuwa meli hiyo ingezama.

"Usisahau tulikuwa na boti 16 za kuokoa maisha na kila moja ilibeba watu 50, na kama zingejazwa zote tungeweza kuokoa watu 800 ambapo tuliokoa 500 tu," alisema.

Nilikuwa nikiingiwa na baridi na kuhisi kuganda taratibu, na kwa neema ya Mungu nilikutana na boti ya kuokoa maisha na wakanivuta ndani - Frank Prentice

Bwana Prentice na wanaume wengine wachache waliamriwa kuchukua biskuti zote ambazo wangeweza kubeba kutoka kwenye chumba cha kuhifadhi. Hadi wakati wanarudi kwenye sitaha, meli ilikuwa katika hali mbaya na hakuweza kusonga mbele tena ili kufikia boti za kuokoa maisha.

Alipokuwa akiharakisha kuvaa jaketi lake la kuokoa maisha, meli ilikuwa inazama kwa kasi ya ajabu na hofu ilikuwa ikiongezeka huku abiria wa daraja la tatu wakijazana kwenye sitaha.

Na kisha meli ya Titanic ikavunjika vipande viwili.

"Ghafla, iliinuka haraka na ungeweza kusikia kila kitu kwa sauti ya juu," alisema.

Bwana Prentice alikuwa ameng'ang'ania ubao huku nusu ya meli iliyogongwa ikipanda juu kutoka majini. Hakuwa na chaguo ila kuachia na kutumbukia ndani ya maji. "Nilikuwa na mkanda wa kuokoa maisha na nikapiga maji kwa nguvu ya ajabu," alisema. Akielea kwenye bahari yenye barafu kati ya "miili kila mahali", alitazama jinsi meli inavyotoweka chini ya maji. Alisema hakutaka kufariki lakini "hakuona fursa kubwa ya kuishi".

Unalala kitandani usiku na tukio zima linakujia tena na tena - Frank Prentice

"Taratibu nilikuwa nikiganda, na kwa neema ya Mungu nilikutana na boti ya kuokoa maisha na wakanivuta ndani," alisema.

Alipotazama huku na kule, alijipata ameketi kando ya Virginia Estelle Clark, eneo ambali halikuwa geni machoni pake kutoka nyuma kwenye sitaha ambapo alikuwa amewasaidia wanandoa wachanga kwa jaketi zao za kuokoa maisha.

Alikuwa amemshawishi Bi Clark kumwacha mume wake Walter nyuma na kuingia kwenye boti ya kuokoa maisha, na kumhakikishia kwamba alikuwa na uhakika wa kumfuata baadaye. Bi Clark alimuuliza Bwana Prentice ikiwa amemwona mumewe. Baadaye ilitokea kuwa alikuwa mmoja wa waliofariki.

Comments

Popular Posts