Historia ya Bodi ya Filamu Tanzania

Historia ya Bodi ya Filamu Tanzania

Historia ya sekta ya filamu nchini inaweza kuelezewa kwa vipindi vitatu, yaani kipindi cha wakati wa Ukoloni (1880 – 1961), kipindi cha Uhuru (1961 – 1990) na kipindi cha Soko Huria (1990 hadi sasa).


Wakati wa ukoloni, filamu zililetwa kwa ajili ya burudani, kwa dhana ya kuwastaarabisha Waafrika na kueneza propaganda kuhusu uwezo wa nchi zao katika masuala ya vita, hususani vita vya kutumia ndege. Aidha, mwaka 1930, Serikali ya kikoloni ilitunga Sheria ya Picha za Filamu, Sura ya 230 (The Cinematograph Ordinance Cap. 230) ambayo iliweka utaratibu wa nani atazame filamu zipi kati ya Wazungu, Waasia na Waafrika. Sheria hiyo iliunda bodi iliyojulikana kama Film Licensing and Censorship Board.


Baada ya uhuru, taasisi binafsi zilijitokeza katika utengenezaji, uzalishaji, usambazaji na uoneshaji wa filamu. Aidha, Serikali ilianzisha taasisi na vitengo ambavyo vilitumika kutengeneza filamu zenye maudhui ya kuhamasisha maendeleo, umoja wa kitaifa na matukio mengine ya kiserikali. Taasisi zilizoanzishwa ni pamoja na Kampuni ya Filamu Tanzania (TFC) mwaka 1968 iliyokuwa na jukumu la kupata urari wa kazi za kitanzania, Taasisi ya vielelezo ya Dar es Salaam (AVI) mwaka 1974, Maktaba ya Filamu iliyoanzishwa mwaka 1972 na Bodi ya Filamu iliyoanzishwa mwaka 1976. Pia, katika kipindi hicho, Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Na. 4 ya Mwaka 1976 ilitungwa.


Katika kipindi cha soko huria, sehemu kubwa ya uzalishaji, uagizaji na usambazaji wa kazi za filamu ulifanywa na sekta binafsi bila kulazimika kupitia katika kampuni ya filamu Tanzania (TFC). Baadhi ya Kampuni zilizokuwa zinajishughulisha na kazi hizo ni Pan-African Film Distributors, United Film Distributors na Anglo-American Film Distributors. Aidha, kuanzia miaka ya 2000, ukuaji wa sayansi na teknolojia umechochea kampuni binafsi za wazawa kupata mwamko wa kuendesha Sekta ya Filamu kibiashara kwa kuzalisha, kusambaza, kuonesha na kufadhili kazi za filamu. Vilevile, kumekuwapo na uanzishwaji wa vyombo vya wadau, vikiwemo Shirikisho la Filamu Tanzania na vyama vinavyounda shirikisho hilo, pamoja na asasi na taasisi binafsi zinazoshughulika na uendelezaji wa Sekta ya Filamu.

Comments

Popular Posts